Tuesday , 1st Dec , 2015

Uongozi wa Klabu ya Azam FC umesema usajili wa mlinda mlango Ivo Mapunda ni wa pekee hivyo hawatasajili tena mchezaji mwingine katika dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufungwa Desemba 15 mwaka huu.

Afisa Habari wa Azam FC Jaffary Maganga amesema, Ivo amesajiliwa kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuomba kufanya mazoezi na klabu hiyo ambapo alionesha juhudi na kocha kumpendekeza asajiliwe katika dirisha Dogo la usajili kutokana na kiwango kizuri alichokionesha katika mazoezi.

Maganga amesema mkataba wa Ivo upo wazi kwa maana hamzuii endapo atapata timu nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza kipato hatokuwa na kipingamizi chochote.

Kwa upande wa sakata lililokuwepo baina ya kiungo mshambuliaji ya Azam FC Brian Majwega aliyeomba kufanya mazoezi na klabu ya Simba, Maganga amesema, wapo katika hatua za mwisho kwa ajili ya mchezaji huyo kuwa mchezaji rasmi wa Simba.

Maganga amesema, Simba wameweza kubaini kuwa ni kweli Majwega bado ana mkataba na Azam FC hivyo wapo katika taratibu za mwisho za kimaandishi kwa upande wa timu ya Azam FC, Simba, klabu yake ya zamani ya KCCA pamoja na wakala wake.