Thursday , 17th Dec , 2015

Baada ya kutinga hatua ya raundi ya tatu ya kombe la FA uongozi wa klabu ya Friends Rangers ya jijini Dar es salaam umelitaka shirikisho la soka nchini TFF kuangalia namna ya kuwaondoa viongozi wa klabu wenye maslahi binafsi kwenye bodi ya ligi.

kikosi cha Friends Rangers katika moja ya mechi ya ligi daraja la kwanza msimu uliopita.

Akizungumza na East Africa Radio katibu mkuu wa klabu hiyo Herry Mzozo amesema ni vyema viongozi wa klabu wasijumuishwe kwenye bodi ya ligi kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakiweka maslahi ya timu zao mbele kuliko kutenda haki.

Mzozo amemtaka waziri mwenye dhamana wizara husika Nape Nnauye kutazama jambo hili kwa kuwa limekuwa kikwazo kwao kupanda kucheza ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Friends Rangers hapo jana imeibuka kidedea kwa kuwachapa wenzao wa kinondoni KCMC kwa penati 6-5 baada ya sare ya kufungana bao 2-2.

Hatua ya tatu ya michuano hiyo itajumuisha vilabu vya ligi kuu sambamba na timu zilizo fanikiwa kushinda michezo yao ya mzunguko wa pili unayohusisha timu 16 kutoka ligi daraja la kwanza na 16 waliyoshinda katika mzunguko wa kwanza..