Jengo la ofisi za Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF.
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetangaza leo Mei 27, 2016 kuanza kwa mchakato wa kuchukua fomu za kugombea uongozi katika Klabu ya Young Africans ya Dar es Salaam inayotarajia kufanya uchaguzi tarehe 25 Juni mwaka huu.
Nafasi zinazogombewa ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wanane wa Kamati ya Utendaji.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Aloyce Komba, fomu zinapatikana katika ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Vilevile utaratibu unafanyika ili fomu ziweze kupatikana katika tovuti ya shirikisho.
Fomu zinapatikana kwa gharama ya Sh 200,000 kwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na Sh 100,000 kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji. Mwisho wa kuchukua fomu ni tarehe 31 Mei, 2016.
Awali baadhi ya wanachama wa klabu ya Yanga na viongozi wa baraza la wazee wa klabu hiyo kwa nayakati tofauti walikuwa wakitaka uchaguzi huo ambao ulikuwa ufanyike tangu miezi 18 iliyopita usogezwe mbele tena kutokana na timu hiyo kutingwa na majukumu mengi ya usajili lakini kubwa ni kutoathiri ushiriki wake katika michuano ya vilabu barani Afrika ambapo Yanga wamefuzu kuingia hatua ya makundi [nane bora] ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika CAF CC.
Nakutokana na hali hiyo wanachama hao wakawa wakipaza sauti zao kushinikiza jambo hilo ili kutoa fursa kwa timu kujikita katika ushiriki wa mashindano hayo ya pili kwa ukubwa barani Afrika jambo ambalo kwa mujibu wa katiba na agizo la baraza la michezo nchini ni wazi kwa sasa baada ya kutangazwa kwa zoezi la utoaji fomu basi mchakato ndiyo umeanza rasmi na hakutakuwa na namna nyingine ya kufanya.