Thursday , 13th Apr , 2017

Mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Chelsea na timu ya Taifa ya Ivory Coast Didier Drogba amejiunga na klabu ya ligi daraja la kwanza ya Marekani Phoenix Rising kama mchezaji na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo.

Didier Drogba

Drogba mwenye umri wa miaka 39, hakucheza soka tangu aachane na klabu ya ligi kuu ya soka nchini Marekani Montreal Impact mwaka uliopita.

Taarifa ya klabu ilisema: "Phoenix Rising Football Club imemtangaza mshambuliaji mkongwe Didier Drogba kujiunga na uwekezaji wa ligi kuu ya soka ya Marekani, na atawekeza zaidi kwa mafanikio ya klabu ya ligi daraja la kwanza".

"Kumiliki timu na kuwa mchezaji kwa wakati mmoja siyo kitu cha kawaida, lakini kinakuwa kitu cha kusisimua. Ni mabadiliko mazuri kwa sababu nataka kuendelea kucheza lakini nakaribia umri wa miaka 40 na ni muhimu sana kwangu kujiandaa na kazi yangu ya baadae". Alisema Drogba.

Drogba alifunga mabao 157 katika mechi 341 alizochezea Chelsea katika kipindi cha 2004 hadi 2012, akishinda mataji matatu ya ligi kuu ya soka nchini Uingereza na taji moja la ligi ya mabingwa Barani Ulaya.