Sunday , 29th Jan , 2017

Mshambuliaji ghali zaidi wa klabu ya Yanga raia wa Zimbabwe, Obrey Chirwa leo ameifungia timu yake mabao mawili muhimu na kuipa kuipa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mwadui FC katika mchezo uliopigwa dimba la Taifa Dar es Salaam

Wachezaji wa Yanga, Chirwa na Msuva wakishangilia bao

Ilikuwa ni kama vile kocha wa Yanga George Lwandamina alipigiwa simu ya siri na kunong'onezwa kuwa anapaswa kufanya mabadiliko, kwani Chirwa amefunga mabao hayo akitokea benchi baada ya mabadiliko ya kumtoa Haruna Niyonzima katika dakika za 60 baada ya Mwadui kuwa wameibana vilivyo Yanga na kuifanya hadi dakika hizo kuwe kukavu.

Chirwa amepachika bao la kwanza katika dakika ya 70 akimalizia mpira uliopanguliwa na golikipa Shaaban Kado kufuatia shuti kali la Saimon Msuva.

Dakika 12 baadaye Chirwa alionesha utulivu wa hali juu ndani ya box la sita, baada ya kupokea pasi nzuri na kufunga kwa utulivu akimchambua kipa Shaaban Kado ikiwa ni dakika ya 82.

Mabadiliko mengine aliyoyafanya Lwandamina kipindi cha pili kabla ya mabao hayo kupatikana, ni kuwatoa Amis Tambwe na Deusi Kaseke na nafasi zao kuchukuliwa na Emanuel Martin pamoja na Said Juma Makapu. Pia katika mchezo wa leo, nahodha wa Yanga Nadir Haroub 'Canavarro' amerejea dimbani kutokana na Dante kuwa majeuhi.

Mwadui ambao muda mwingi walicheza kwa kujihami zaidi, walianza kufunguka na kujaribu mashambulizi, lakini mashambulizi yao hayakuwa na matumaini yoyote.

Hadi mwisho wa mchezo, Yanga 2, Mwadui 0 na sasa Yanga ndiyo kinara wa ligi hiyo kwa kufikisha point 46 ikiipiku Simba yenye pointi 45 baada ya kuchapwa na Azam siku ya jana.

Chirwa anaongeza ushindani katika mbio za ufungaji bora, ambapo hadi sasa ana mabao 7 nyuma ya John Bocco mwenye mabao 8 na vinara Kichuya, Tambwe na Msuva wenye mabao 9 kila mmoja.

Katika mchezo mwingine uliopigwa leo, Majimaji imepata ushindi wa bao 1-0 ikiwa ugenini dhidi ya Ndada FC