
Katika mchezo huo, Twiga Stars itautumia nafasi hiyo kumuaga mshambuliaji wake wa siku nyingi Estha Chaburuma ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa Twiga Stars na sasa anastaafu rasmi kucheza mpira wa miguu.
Akizungumza na East Africa Radio, Ester amesema ameamua kustaafu soka ili kuweza kuwapa nafasi wachezaji vijana wengine wanaochipukia katika kikosi hicho.
Ester amesema, katika kipindi chake cha soka atakumbuka mechi ya kuwania kufuzu katika fainali za Afrika ambapo walifanikiwa kufanya vizuri huku akiwa na mchango mkubwa katika ushindi wa mechi hiyo waliyocheza dhidi ya Ethiopia ambapo walianzia ugenini na kumalizia nyumbani Tanzania.
Ester amesema, amewataka vijana walio ndani ya timu ya taifa kuonesha nidhamu pamoja na kujituma ili kuweza kufika mbali zaidi katika malengo waliyojiwekea kwani anaamini timu ni nzuri ila wachezaji waongeze bidii ili kuweza kufanya vizuri zaidi katika michezo iliyo mbele yao.
Ester amesema, uongozi wa shirikisho la soka nchini TFF umemteua kuwa katika benchi la ufundi lakini katika kozi za makocha zitakazokuja atasoma ili aweze kuwa kocha na kuweza kurudi tena kwa ajili ya kufundisha.
Upande wa timu ya taifa ya Malawi tayari imewasili jana jioni jijini Dar e salaam ikiwa na kikosi cha wachezaji 20 pamoja na viongozi nane ambapo jioni hii kinaendelea na mazoezi katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.