Akizungumza na East Africa Radio, makamu mwenyekiti wa CHABATA, Simon Jackson amesema, kila kanda itachagua wachezaji 20 watakaokuwa na kiwango kikubwa ambao wataungana pamoja na kuchuana katika mashindano ya Taifa yaliyopangwa kufanyika Julai mwaka huu jijini Dar es salaam.
Simon amesema, licha ya kugawa mashindano ya mikoa katika kanda lakini pia Zanzibar imepangiwa kutafuta waendesha baiskeli 40 ambao wataungana na wengine 120 wa kanda za Tanzania bara.
Simon amesema, kamati ya ufundi ya CHABATA ililazimika kugawa mashindano hayo katika kanda wakiwa na lengo la kuwapa nafasi kubwa ya kuwapata wachezaji kwa kila mkoa lakini inakuwa rahisi kuzisimamia kanda hizo kuliko kila mkoa kufanya mashindano yake.
Waendesha baisikeli wote 160 watashindana kwa pamoja na wale watakaofanya vizuri watapewa mazoezi hadi watakapoitwa katika kambi ya timu ya taifa itakayoandaliwa na Serikali kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya kwenda nchini Congo Brazaville.