Saturday , 7th May , 2016

Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans Van Der Pluijm amewaanzisha kwa pamoja washambuliaji Malimi Busungu na Amissi Tambwe kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya Esperanca.

Wachezaji wa Yanga Salum Telela [kushoto] na Malimi Busungu [kulia]

Mchezo huo unaochezwa jioni ya leo katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam na unachezeshwa na marefa kutoka Ghana, ambao ni Joseph Odartei Lamptey anayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera David Laryea na Malik Alidu Salifu, wakati Kamisaa ni Asfaw Luleseged Begashaw kutoka Ethiopia.

Busungu amechukua nafasi ya mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma ambaye anatumikia adhabu ya kadi za njano mfululizo alizopewa kwenye mechi dhidi ya Al Ahly ya Misri mwezi uliopita.

Aidha, kwa kukosekana kwa Mzimbabwe mwingine, kiungo Thabani Kamusoko, Pluijm amewaanzisha viungo Salum Telela na Haruna Niyonzima.

Deus Kaseke anacheza kama kiungo wa pembeni, ambaye atakuwa na jukumu la kuwa katikati muda wingi, wakati Simon Msuva anacheza wingi ya kulia.

Safu ya ulinzi ya Yanga inaendelea kuwa chini ya kipa Deo Munishi ‘Dida’, beki wa kulia Juma Abdul, Oscar Joshua kushoto na kati Kevin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Kikosi kamili cha Yanga ni; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Malimi Busungu, Amissi Tambwe na Deus Kaseke.

Katika benchi wamo; kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Mwinyi Hajji, na washambuliaji Geoffrey Mwashiuya, Paul Nonga na Matheo Anthony.