Wednesday , 20th Jul , 2016

Baraza la michezo nchini BMT limewataka wanachama wa Chama cha Judo nchini JATA wenye sifa za kugombea uongozi ndani ya chama hicho kuendelea kujitokeza kwa ajili ya kuchukua fomu za uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 06 jijini Dar es salaam.

Afisa habari wa BMT Najaha Bakari amesema mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu za uchaguzi ndani ya chama hicho ni Agosti mosi mwaka huu na mpaka sasa ni watu wawili pekee waliojitokeza kwa ajili ya kuchukua fomu za ugombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho na bado watu wanahitajika kwa ajili ya kuhakikisha wanapatikana viongozi ambao watauendeleza mbele mchezo huo hapa nchini.

Najaha amesema, nafasi zinazogombewa ndani ya chama hicho ni nafasi ya Rais, Makamu wa Rais, Katibu, Katibu mkuu msaidizi, muweka hazina, wakurugenzi wa kamati za waamuzi, ufundi, fedha na masoko, elimu na michezo, kujitolea na ustawi.

Kwa upande mwingine Najaha amesema, wajumbe wote watakaohudhuria mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba ya ndani ya chama hicho utakaofanyika siku moja kabla ya uchaguzi wanatakiwa kufika wakiwa na barua ya utambulisho pamoja na cheti cha usajili ili kuwawezesha pia kupiga kura ndani ya chama hicho.