Thursday , 14th Apr , 2016

Baraza la michezo nchini Tanzania BMT limesema shughuli zote za vyama vya ngumi za kulipwa nchini zitakuwa zikiratibiwa na BMT lengo likiwa ni kuwa na chombo kimoja kutakachokuwa kikiratibu ngumi za kulipwa nchini.

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT Mohamed Kiganja amesema, hapo awali kila mtu alikuwa akijichukulia jukumu na kuendesha shughuli za mchezo wa ngumi bila kufuata taratibi zozote zinazotambulika kiserikali.

Kiganja amesema, wameunda kamati ambayo kinawajumbe ambao wametoka kila taasisi ambapo wajumbe hao ni Yahaya Poli, Chaurembo palasa, Nemes Kavishe na Onesmo Ngowi wote kutoka TPBC, Yassin Ustaadh kutoka TPBO, Habibu Kinyogoli, Emmanuel Mlundwa kutoka PST.

Kiganja amesema, vyama hivyo vitafuata sheria za BMT na za ngumi zilizopo na hata shughuli zao za misafara yote ya nje kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya ngumi kwanza kamati iliyoteuliwa lazima ijue na ipeleke taarifa zote BMT kwa kila alichokifanya nje ya nchi.

Kwa upande wake Mjumbe kutoka TPBO ambaye pia ni Rais wa shirikisho la ngumi za kulipwa nchini TPBO Yassin Ustaadh amesema, BMT imechelewa kuanzisha mfumo huo ambao ndio unaotumika Duniani kote na utasaidia mabondia nchini kwani katika nchi mbalimbali mchezo wa ngumi za kulipwa ni biashara kati ya bondia na Promota yaani muandaaji na vyama vinakuwa kama wasimamizi ambao wanatoa wataalamu wa kuchezesha mapambano.

Ustaadh amesema, chombo kilichoundwa hakitamtetea mtu bali kitamuwajibisha kila mtu anayehusika hususani waandaaji matapeli ambao wamekuwa wakiendesha mchezo huo kwa kuwapandisha mabondia ulingoni na baada ya kumaliza kazi wanakwepa kuwalipa kama alivyokubaliana.