Mmoja wa washiriki wa shindano la Baiskeli nchini akishangilia ushindi wake.
Ni wazi sasa Chama chenye dhamana kubwa yakusimamia mchezo wa baiskeli nchini Tanzania CHABATA kimeonyesha nia ya dhati na thabiti kabisa kwa mwaka huu kuhakikisha inarejesha hadhi ya mchezo huo ambayo imepotea na kusababisha hata mashindano mbalimbali yanayoandaliwa kukosa msisimko wakutosha.
Moja ya mikakati ya CHABATA ni pamoja na kutoa agizo ama wito kwa vyama vya mikoa yote na vyama shiriki vyote vya mchezo wa baiskeli kote nchini kujifunga kibwebwe na kuhakikisha mchezo huo unapiga hatua na kusonga mbele hasa kwa kuanziasha mashindano mengi ya ndani kwa lengo la kupata wachezaji bora ambao wataunda timu imara na zenye ushindani toka katika mikoa yao ambao baadae watashiriki katika mashindano ya kanda na baadae ya taifa ambayo yatatoa kikosi bora cha taifa kitakachoshiriki michuano mbalimbali itakayofanyika wakati wowote kwa msimu husika.
Na kwakuanzia mwenyekiti wa chama cha mchezo wa baiskeli nchini Tanzania CHABATA Said Kengere [SK] ametangaza rasmi na kuthibitisha kuwa Tanzania itashiriki michuano maarufu ya kimataifa ya mbio za baiskeli za Rwanda ijulikanayo kama Tour de Rwanda 2016 ambayo mwaka jana hawakushiriki baada ya kukosa mwaliko hasa kutokana na kile alichodai kuwa Tanzania ilionekana kuwa bado changa na hivyo kuonekana kutoweza kumudumu mikikimikiki na ushindani na timu zenye uzoefu kimataifa.
Aidha Kengere kwa kuliona hilo ameona na vyema kwa vyama vyote na vyama shiriki vya mchezo wa baiskeli na pia vilabu kushirikiana kuendesha mashindano mbalimbali ya ndani ili kupata timu bora ambazo zitashindana na baadae kuunda kikosi bora na imara cha taifa ambacho kitashiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na kutoa ushindani wa kweli.
Akimalizia Kengere amesema CHABATA imeamua kuweka mikakati ya dhati kabisa ya kuinua mchezo wa baiskeli na kwa mwaka huu wamejipanga na wako tayari kwa ushiriki wa michuano hiyo mikubwa ya Rwanda ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo mwezi Novemba.