Wachezaji wa timu ya Azam na Yanga wakichuana katika moja ya michezo iliyozikutanisha timu hizo.
Marekebisho ya mechi mbili za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara VPL zinazozihusu timu za Azam na Yanga zilizopangwa kufanyika mapema wki ijayo, zimeahirishwa.
Mechi hizo ni kati ya Mtibwa Sugar na Azam FC uliopangwa kupigwa siku ya Jumanne ya Machi 22 Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na ule wa mabingwa watetezi wa ligi hiyo timu ya Yanga SC dhidi ya Mwadui FC uliopangwa kupigwa siku ya Jumatano ya Machi 23, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwaka huu.
Sababu za kufutwa kwa mechi hizo ni kupisha ratiba ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 2017 na pia kutoa fursa kwa vilabu hiyo ambavyo ndiyo wawakilishi wa Tanzania bara katika michuano ya shirikisho la soka barani Afrika CAF kwa ngazi ya vilabu barani Afrika.
Taifa Stars itakuwa na mchezo wa kufuzu kwa michuano ya mataifa ya Afrika AFCON Kundi G dhidi ya Chad mjini N’jamena Machi 25,na baadae timu hizo kurudiana Machi 28, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na baada ya mechi za mwishoni mwa wiki za michuano ya klabu barani, Afrika wachezaji wa Stars wanatarajiwa kukusanywa Jumapili kabla ya safari Jumanne kuelekea Chad.
Yanga SC baada ya ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR Jumamosi mjini Kigali, watarudiana na timu hiyo ya jeshi la Rwanda Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na Azam FC baada ya kushinda 3-0 mjini Johannesburg, Afrika Kusini dhidi ya wenyeji Bidvest Wits katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika, watarudiana na timu hiyo Jumapili, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Pamoja na hayo, Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara VPL inatarajiwa kuendelea leo na kesho na mwishoni mwa wiki.
Azam FC wataikaribisha Stand United kesho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa Stand United ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza mechi 22 haina nafasi ya ubingwa na wala haimo kwenye hatari ya kushuka daraja, hivyo huo ni mchezo ambao hauwatii ‘presha’ hata kidogo.
Lakini Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi zake 47 za mechi 20 katika mbio za ubingwa dhidi ya Yanga yenye pointi 50 za mechi 21 na Simba iliyo kileleni kwa pointi zake 54 za mechi 23 – inahitaji ushindi ili kujiimarisha.
Simba itashuka tena dimbani Jumamosi kucheza na Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kwingineko ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kusaka tiketi ya kucheza michuano ya mataifa ya Afrika kwa wanawake timu ya taifa ya soka ya wanawake Twiga Satars inatarajiwa kusafiri siku ya Ijumaa kuelekea nchini Zimbabwe kwa ajili ya mchezo wake wa marudiano wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Cameroon.
Kikosi cha Twiga Stars kinaendelea na mazoezi katika uwanja wa Karume chini ya kocha mkuu, Nasra Juma kujiandaa na mchezo huo muhimu ili kuweza kusonga mbele katika hatua inayofuata.
Kuhusu maendeleo ya kambi, kocha Nasra Juma amesema vijana wake wanaendela vizuri, wamekua wakiendelea na mazoezi tangu baada ya mchezo wa awali na ana imani watafanya vizuri katika mchezo wa marudiano.
Twiga Stars inahitaji ushindi katika mchezo huo wa marudiano utakaochezwa Jumapili, Machi 20 katika uwanja wa Rufalo uliopo jijini Harare ili kuweza kufuzu kwa hatua ya pili ya michuano hiyo.