Tuesday , 30th Jan , 2018

Kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho leo, klabu ya soka ya Azam FC imesema ratiba ya mechi yao kuchezwa 8:00 mchana ndio changamoto ambayo timu hiyo itakutana nayo.

Azam FC leo itashuka kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro kukipiga na klabu ya Shupavu FC ikiwa ni mchezo wa hatua ya 32 bora. Mchezo huo unatarajiwa kuanza mchana kitendo ambacho Azam wameeleza kitawapa taabu kidogo.

Msemaji wa timu hiyo Jaffary Idd akiwa Morogoro mchana huu amesema timu yao imejindaa na mchezo huo, lakini suala la mechi kuchezwa mchana ndio limebaki kama changamoto kutokana na timu hiyo kuzoea kucheza usiku au jioni.

Kwa upande mwingine Jaffary amesema wao kama Azam FC hawaifahamu timu ya Shupavu FC lakini hiyo haiwafanyi waipuuze kwani nguvu zao zote wamewekeza kwenye michuano hiyo pamoja na ligi kuu.