Saturday , 5th Jan , 2019

Kikosi cha Alliance FC cha Jijini Mwanza kimeshindwa kutumia  vyumba vya kubadilisha nguo kwa madai ya vyumba hivyo kupuliziwa dawa ambazo si afya na ambazo zingepelekea kuwaathiri.

Alliance FC

Imeshuhudiwa timu hiyo ikifanya 'Warm up' (maandalizi kabla ya mchezo) na kisha kurejea kwenye gari lao kwaajili ya kujiandaa kuingia uwanjani kupambana na Mbao FC ya Jijini humo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Alliance FC, Yusuph Budodi amesema kuwa wameshindwa kuingia vyumbani baada ya kubaini kupuliziwa dawa ambazo zinaweza kuwaathiri.

"Ni kweli hatujaingia vyumbani kwa sababu kuna harufu nzito,wamepulizia dawa sasa tutapelekaje wachezaji angali hali ya hewa ni mbaya hivyo?," amehoji Budodi.

Alliance FC imekuwa na muendelezo mzuri wa michezo yake ya ligi kuu baada ya kuajiri kocha mpya ambaye alikuwa kocha wa zamani wa Mbao FC, Malale Hamsini. 

Ikiwa imeshinda michezo mitatu kati ya sita ya mwisho, huku ikipoteza miwili na kutoka sare mchezo mmoja. Inakamata nafasi ya 14 mpaka sasa katika msimamo wa ligi, ikifanikiwa kujinasua kutoka mkiani.