Wednesday , 28th Nov , 2018

Jaffar Kibaya ni jina ambalo kuanzia jana limetawala vinywani mwa wapenda soka nchini baada ya kuifungia klabu yake ya Mtibwa Sugar mabao matatu kwenye ushindi wa 4-0 iliopata dhidi ya Northen Dynamo ya Ushelisheli kwenye kombe la shirikisho barani Afrika.

Mchezaji wa Mtibwa Sugar Jaffary Kihimbwa akiwatoka wachezaji wa Nothern Dynamo.

Leo Novemba 28, 2018 Kibaya amefanya mahojiano maalum na www.eatv.tv na kusema kuwa hakuwa anajua chochote kuhusu rekodi za michuano hii mpaka mchezo ulipomalizika ndipo alipofahamu kuwa mabao yake yameweka rekodi za wachezaji wakubwa wa Simba na Yanga.

''Baada ya mechi wachezaji wenzangu na viongozi walianza kunipongeza kuwa nimeweka rekodi ndio nikawauliza rekodi gani wakanieleza nimefikia rekodi ya Joseph Kaniki ambaye ndiye alikuwa mchezaji wa Mtibwa Sugar kuwahi kufunga mabao mengi kwenye michuano ya kimataifa'', amesema Kibaya.

Hata hivyo Kibaya amewasifu walimu wake chini ya kocha mkuu Zuberi Katwila, kuwa walifanya maandalizi mazuri ya mechi kwa kuzingatia wapinzani wao na ndio maana waliibuka na ushindi huo.

Joseph Kaniki ambaye aliyeichezea Mtibwa Sugar na baadaye kung'ara na Simba pamoja na Mrisho Ngassa anayechezea Yanga hivi sasa, ndio wachezaji pekee wa Tanzania kufunga mabao matatu (Hat-trick) katika michuano ya klabu barani Afrika hivyo Jaffary Kibaya ameungana nao kwenye rekodi hiyo.

Kuelekea mchezo wa marudiano ambao utapigwa kati ya Disemba 4 na 5, Kibaya amesema wameshawasoma wapinzani wao hivyo anaamini watakwenda kufanya vizuri ugenini na kusonga mbele.