Thursday , 2nd Jun , 2016

Kiongozi wa zamani wa klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kuwa wanachama wengi wa klabu hiyo wamemfuata kumuomba agombee katika uchaguzi wa Juni, lakini anasikitika hataweza kutekeleza ombi lao.

Amesema kuwa watu wamemtumia meseji, wamempigia simu na wengine wamemfuata ofisini kwake kumuomba agombee, tena wengine wametaka kumpelekea fomu nyumbani au ofsini kwake.

Aidha, amesema aliamua kujitoa kwenye uongozi wa Yanga kutokana na kubanwa na shughuli zake binafasi mwaka jana na kwamba hadi sasa hakuna kilichobadilika.

"Nilimuomba Mwenyekiti aniondoe kwenye uongozi baada ya kubanwa na shughuli binafasi ikiwemo masuala ya familia, na hadi sasa hakuna mabadiliko, kwa sababu zile zile, sitagombea" amesema Bin Kleb.

Hata hivyo, Bin Kleb amesema kuwa pamoja na kujitoa kwenye uongozi wa klabu, lakini ameendelea kushirikiana na uongozi uliopo madarakani na kutoa michango yake ya hali na mali.

"Ninashirikiana nao vizuri na wao wanajua. Hata baadhi ya wanachama walio karibu sana na timu wanajua kwamba bado ninasaidia Yanga. Vivyo hivyo, hata kwa uongozi ujao, nitaendelea kusaidia Yanga nikiwa nje ya uongozi,"amesema Bin Kleb.

Bin Kleb amewashukuru wanachama wa Yanga kwa kuendelea kumuamini na kwa heshima wanayompa, lakini anawaomba radhi kwamba hataweza kwa sasa.

Uchaguzi wa Yanga unatarajiwa kufanyika Juni 11 mwaka huu na leo wanachama wanatarajiwa kuanza kuchukua fomu Makao Makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam.