Eden Hazard
Mchezaji huyo ambaye amekuwa akihusishwa na tetesi kadhaa za kujiunga na mabingwa watetezi wa klabu bingwa Ulaya, Real Madrid amesema kuwa hakutakuwa na shida yoyote endapo atashindwa kujiunga na miamba hiyo.
Miezi ya hivi karibuni, mwenyewe Hazard alishawahi kusema kuwa anapenda siku moja acheze katika ligi kuu ya nchini Hispania 'La Liga', kitu ambacho kimeleta mashaka juu ya uwepo wake katika klabu ya Chelsea msimu ujayo.
"Ni kwamba, nisipokwenda Hispania, haina tatizo, ninawapenda sana mashabiki wangu na nafikiri mashabiki wananipenda. Kitakachotokea hapo mbeleni nitakuwa na furaha pia, ni hilo", amesema Hazard.
Nyota huyo ambaye ameshinda mataji mawili ya ligi kuu nchini Uingereza (PL), ataiongoza Chelsea itakapopambana na Manchester United wikiendi hii, mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Stamford Bridge.
Hazard amekuwa na kiwango bora sana tangu kuanza kwa msimu huu, akifunga mabao 7 mpaka sasa katika ligi hiyo na kuisaidia klabu hiyo kukwea hadi nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kwa alama zake 20.


