Tatizo hilo limeelezwa kuathiri kwa kiasi kikubwa afya za waathirika kwa kujaribu kutumia njia mbadala kupata tiba, ikiwemo Kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo sasa hivi matangazo yake yamejaa kila kona, dawa ambazo huleta madhara makubwa ya kuupelekea mwili kwa anayetumia kukosa muelekeo.
Hayo yamebainishwa na Mfamasia wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto na Mtaalamu wa Afya ya Jamii Edgar Basheka katika mahojiano na East Afrika Radio leo asubuhi katika kipindi cha East Africa Breakfast.
Mtaalam huyo ameendelea kuelezea kwamba kitendo cha vijana wa kiume kutumia dawa za kuongeza nguvu kuna wapelekea kukosa kujiamini anapokuwa na mwenzake, kwa kuhisi hatamridhisha mpaka pale atakapotumia dawa hizo ndio hali ya kujiamini inarejea.
Mtaalamu huyo amesema madhara ya kutumia dawa yasiyofuta utaratibu, anayetumia anaweza kuongeza dozi au kupunguza hivyo kuchelewesha kupona kwa tatizo au kuleta madhara makubwa zaidi.
Aidha mtaalam huyo wa masuala ya afya ameendelea kufafanua kwamba kutumia dawa bila ya kufuata ushauri wa Daktari, kunaongeza tatizo kwa kuwa dawa zinazotumika hazijafuata utaratibu, kwani hakuna dawa isiyokuwa na madhara, na kuwashauri vijana kuacha mara moja .
“Kutumia dawa kunaleta usugu mwilini, mgonjwa angeweza kutibiwa kwa elfu ishirini, sasa atatibiwa kwa laki nane kutokana na kujiongezea tatizo, mgonjwa lazima afike kituo cha Afya apate ushauri pamoja na maelekezo maalumu, nawashauri vijana waache kutumia dawa hizo waende katika vituo vya Afya kwa ajili ya ushauri", amesema Edgar Basheka
"Dawa hutolewa kwa kufuata umri na uzito, sasa unatumiaje dawa usiyojua, wengi huwa wanatumia dawa kwa kutofuata utaratibu, unapoenda kwa mtaalamu anajua akikupa dawa anafahamu kuwa kuna madhara unayapata ya muda mfupi ila tatizo lako kubwa linapona, hivyo ni vyema waache kufanya hivyo”, ameendelea kusema Edgar Basheka
Kutokana na kauli hiyo ya mtaalam, ni vyema ukaenda kumuona daktari na kumuelezea tatizo lako ili aweze kukusaidia, badala ya kujichukulia uamuzi ambao huenda ukakuongezea tatizo zaidi.