Hussein Bashe akiwa Kikaangoni
Bashe ametoa ushauri huo, alipokuwa KIKAANGONI ya ukurasa wa Facebook ya EATV, ambapo amesema kuwa serikali ni lazima ichukue hatua madhubuti kwa wamiliki wa mabasi ambayo yanasababisha ajali kwa kuwatoza faini pamoja na nyingine kuzifungia ili iwe fundisho kwa wengine.
“Mimi binafsi mwaka huu nimepoteza ndugu zangu wawili kwa ajali ya barabarani kutokana na uzembe wa hali ya juu wa madereva, na matukio haya yanapotokea mabasi yanashikwa na baada ya muda yanapakwa rangi nyingine na jina la kampuni linabadilishwa kazi inaendelea kwa namna hii hatuwezi kumaliza tatizo la ajali” Amesema Bashe.
Mbunge huyo amekwenda mbali zaidi na kutoa mfano wa vyombo vya habari ambapo , mwandishi akiandika habari yenye utata, mtu wa kwanza anayewajibishwa ni mmiliki wa chombo husika hivyo na kwa wenye kampuni za magari ya usafiri ikiwa hivyo itasaidia.
Aidha katika hatua nyingine Mbunge huyo akijibu swali kuhusu baadhi ya wabunge wa CCM kuitetea serikali kwa kila jambo, amesema si kweli wabunge wa CCM hutetea kila jambo linaloletwa na serikali bali kuna mambo huletwa na serikali na huyakataa kama yana utata.