Makundi matano yaliyoingia robo fainali leo yakiwa katika picha ya pamoja.
Usahili wa mwisho wa Dance 100% 2015, umekamilishwa katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni jijini Dar es Salaam, muamko mkubwa wa makundi yapatayo 28 kutoka ndani na nnje ya mkoa yakiongezea ushindani na burudani zaidi katika michuano hiyo kuelekea kupata makundi mengine 5 yatakayoshinda uchaguzi.
Katika michuano ya leo, Wazawa Crew, The Best, Quality Boys, Majokeri na kundi la wasichana la Cute Babies waliweza kuwashawishi majaji na kuweza kujivunia alama nyingi zaidi zilizowawezesha kushinda nafasi ya kuingia robo Fainali ya Dance 100% 2015.
Wakizungumza baada ya kukamilika kwa usahili, Jaji wa Dance 100% 2015, Shetta amesema kuwa amefurahishwa kuona madansa wamejipanga zaidi, akitarajia mchuano mkali hatua inayofuata kutokana na makundi yote yaliyopita kuwa na uwezo mkubwa, wakati Jaji Queen Darleen akitoa wito kwa Madansa kuwa wepesi kuwahi nafasi za Usahili wakati mwingine kutokana na ushindani mkali wa leo kusababisha makundi mengine kupoteza nafasi kwa kukosa alama chache sana.
Jaji Super Nyamwela ambaye pia ni Dansa mkongwe, ameleeleza kufurahishwa kwake na namna makundi yalivyoonyesha kujipanga leo, na kuwapatia nafasi ya kuchagua vipaji bora zaidi, akifananisha usahili huo kama fainali ya mashindano kutokana na mchuano mkali ulioonyeshwa.
"Usahili huu uliofanyika hapa Leaders Club, umekuwa ni mkubwa zaidi, na kwa kuthibitisha ukubwa wa mashindano haya, kumekuwa na makundi yaliyosafiri kutoka mikoani Arusha na Mbeya kuja kushindana, japokuwa ushindani ulikuwa mkali sana na hawakuweza kupita, dalili inayoashiria hatua inayofuata itakuwa ni yenye msisimko zaidi", Alisema Happy Shame, Mratibu wa michuano hiyo kutoka EATV.
Makundi mwengine ambayo yameshiriki katika usahili leo ni Best Plan, A Town Dancers kutoka Arusha, Boko Young Talent, The Quest Crew, TNT, Tatanisha, DMX, House of Kinetix, Majokery, Sababisha, The World Of Champions, Makaba Crew, Hamadombe, Mazabe Powder, Snap Boys Crew, Bustani Dancers, TGE Hardware, Best love, Chipukizi Dancers, Danger Boys, Butterfly kutoka Mbeya, Bata Boys na Fresh Crew.
Kujionea yote yaliyojiri leo, usisahau kutazama shoo ya Dance 100%, Jumamosi ijayo saa 12:30 jioni EATV pekee.
Dance 100% 2015 inaletwa kwako na EATV na East Africa Radio na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania na Coca Cola, Kinywaji rasmi cha Dance 100% kwa mwaka huu.