Monday , 14th Dec , 2015

Msanii Kala Jeremiah amesema pamoja na kuoneka kwenye harakati za kampeni kwenye uchaguzi uliopita, lakini hafikirii kuwa mwanasiasa ingawa anapenda kuwa kiongozi wa wananchi.

Kala Jeremia ameyasem hayo East Africa Radio alipokuwa akitambulisha wimbo wake mpya wa Malaika kwenye kipindi cha Planet Bongo, na kukiri kuwa kuna watu walishawahi kumshawishi agombee nafasi ya uongozi kwenye siasa.

“Nimeshaombwa sana kugombea ubunge na wanasiasa wenyewe pamoja na wananchi walishawahi kutaka nigombee, wakiwa wanaamini ndani yangu nina sifa ya uongozi”, alisema Kala.

Pamoja na hayo Kala amesema hapendi kuwa mwanasiasa kwani iwapo ataingia kwenye siasa atalazimika kufuata yale ambayo wanasiasa wanayafanya, pia itamlazimu kuwa kiongozi wa watu wachache kutoka jimboni kwake.

“Kingine nitahudumia watu wachache wa jimbo tofauti na muziki wangu, muziki nahudumia raia wengi nchi nzima, hiyo ni sawa na kumaliza chuo kikuu alafu narudi darasa la saba B.”, alisema Kala.

Pia kala Jeremia ameongelea kasi ya Rais Magufuli ya kuongoza taifa na kufuta mianya ya rushwa na ufisadi, na kusema kuwa anavutiwa na utendaji wake wa kazi, kwani ndiyo moja ya mabadiliko waliyokuwa wakiyahuniri wakati wa kampeni, ila haamini kama mawaziri wake wataweza kwenda na kasi hiyo.

“Tumepata Rais ambaye nilikuwa namfikiria kichwani, tulikuwa tunapigana tunataka mabadiliko ndio haya aliyokuja nayo Magufuli, ila sijui kwa mawaziri wake kama wataweza kwenda na kasi yake”, alisema Kala Jeremiah.