Friday , 6th Nov , 2015

Msanii mkongwe kutoka pande za Temeke Inspector Haroun amesema watayarishaji wa muziki wa sasa hawana ushirikiano kama zamani, kitu kilichofanya muziki wa zamani uwe bora kuliko wa sasa.

Inspector Haroun ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kueleza kwamba kwa sasa watayarishaji (Producers) wamekuwa wengi na wanafanya kazi kwa kurahisisha.

"Zamani Producer Mj anatembelewa na Enrico, anatembelewa na Bizman, anatembelewa na P.Funk, wanaenda pale hebu msikilize Inspector bwana amechana kwenye hii ngoma unamuonaje, anakuja mtu mwengine anatoa mawazo ya mastering, studio injinia wanakutana pale, lakini sa hivi mtu ameshapata PC yake moja ana monitor anaenda kununua mic, anaweka soft ware ana fruit roops pale basi imetoka ana studio", alisema Inspector.

Inspector aliendelea kwa kusema kwamba siku hizi studio zimekuwa nyingi, hivyo imepelekea kupoteza kwa ubora wa muziki.

"Siku hizi studio zimekuwa kama mdibwa, kila mtu producer, hiyo kidogo inapoteza muziki wetu, sisemi kwamba maproducer wapya wanafanya vibaya ila najaribu kutoa maoni yangu na mtazamo wangu wa bongo fleva inapoelekea", alisema Inspector.