Wednesday , 10th Oct , 2018

Msanii wa Bongofleva, Baraka the Prince ameshindwa kuachia ngoma zake nne alizopanga kuzitoa leo kutokana na msiba wa 'producer' Pancho Latino, ambaye amefariki jana kwenye ajali ya maji kisiwa cha Mbudya kilichopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kushoto ni 'Producer' Pancho Latino akiwa na Baraka the Prince.

Akiongea na www.eatv.tv Barakah amesema kuwa kuachia ngoma hizo leo ni kukikosea kiwanda kizima cha muziki wa Bongofleva pamoja na Pancho mwenyewe ambaye amewahi kufanya naye kazi ambayo bado haijatoka.

''Pancho alikuwa ni mtu wa karibu sana na mimi nimefanya naye kazi nyingi lakini pia tulikuwa na ukaribu sana tunashauriana vitu vingi na mipango mingi pia, naona kama damu yangu imeondoka kwahiyo siwezi kuachia ngoma nitajikosea sana'', amesema Barakah.

Mkali huyo ambaye ngoma yake ya mwisho kuachia ilikuwa ni 'SINA' ambayo alimshirikisha Madee, amesema kuna ngoma amemshirikisha AY  ambayo katika  'Mixing' na 'Mastering' imefanywa na Pancho pamoja na Harmy B.

Pia amefunguka kuwa mara ya mwisho kuwasiliana na Pancho ilikuwa ni wiki kadhaa zilizopita ambapo yeye alikuwa nje ya nchi lakini Pancho alimtumia ujumbe kupitia DM ya Instagram akimwambia ana 'Beat' ambayo ingemfaa lakini hajafanikiwa kuipata mpaka producer huyo anafariki.