
Rais Magufuli akiwa na Shilole upande wa kulia
Shilole ametoa ufafanuzi huo leo asubuhi kupitia ukurasa wake wa kijamii baada ya kuenea 'video clip' iliyokuwa ikimuonyesha akiongea lugha ya ughaibuni 'kiingereza', akimualika Rais Dkt. John Magufuli kuhudhuria katika mgahawa wake ili kusudi aweze kuonja mapishi yake pamoja na kuomba msaada wa watoto wake katika kupata elimu bora.
"Niombe radhi kwa mlionielewa tofauti mimi huwa si-fake maisha naishi maisha yangu, sina utajiri huo kama mlivyonisema hata nyumba niliwaambia nimejenga kwa kujiwekea kidogo kidogo kama mama ntilie na mwanamuziki, ndio maana nilipofikia hatua fulani nikaona ni vizuri ku-share na nyie ili muone nguvu ya 'support' yenu inavyonipa maendeleo",ameandika Shilole.
Pamoja na hayo, Shilole ameendelea kwa kusema "nilichokiomba juzi kwa baba Magufuli ni 'support' na ufadhili wa wanangu kuendelezwa katika vipaji na taaluma wanazopenda kusoma. Mimi napambana sana kuwasomesha lakini pia natamani wapate kitu zaidi ya nachoweza kuwapatia, hivyo nikaona ni kwanini nisiweke kilio changu kwa Mheshimiwa kwasababu elimu kwa watoto wa kike ni moja ya mambo ambayo naamini anayasimamia vema".
Mbali na kauli hizo, Shilole ni miongoni mwa wasanii wa kike nchini wanaopambana usiku na mchana, katika kuhakikisha anajipatia riziki kupitia maarifa aliyokuwa nayo na nguvu zake na kumfanya awe tofauti na wanawake wengine ambao wamekuwa wakisubiria pesa za mahitaji kutoka kwa wanaume zao.