
Bounako ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kwamba kundi hilo bado linaendelea na harakati, na wameshafanya kazi ambazo bado hazijatoka.
"N2N Soldiers ipo na mawasiliano yapo kama kawaida, bado tunafanya harakati na kuna track kama mbili tumefanya", alisema Bounako.
Bounako ameendelea kwa kusema kwamba kundi hilo kwa sasa linahitaji uongozi ambao utawasimamia kazi zao, na kuacha kujiendesha lenyewe kama walivyokuwa kipindi cha nyuma.
"N2N Soldiers inahitaji management kwa sasa, hatuwezi kwenda kisela kama zamani, na iwapo mtu atatokea sisi tuko tayari muda wowote", alisema Bounako.
Pamoja na hayo Bounako amewataka mashabiki kuwaunga mkono na kuwa wazalendo, kwani bila mashabiki wao kama wasanii hawataweza kufanikiwa katika harakati zao.
"Mashabiki watupe support, watuunge mkono wawe wazalendo, kama unavyojua wao ndio mashabiki na bila mashabiki hatuwezi kufika", alisema Bounako.
Pia Bounako amesema kwa muda wote ambao alikuwa kimya alikuwa akifanya kazi mgodini kwani yeye ni mchimbaji wa madini ya Tanzanite yaliyopo Mererani na kusema kwamba alipojiingiza kwenye kazi hiyo ilikuwa changamoto kubwa kwake kutokana na mazingira ya mgodini.
"Unajua mi nazama chini, siku ya kwanza ilikuwa ni suprise kwangu, nilikuwa na uoga lakini nikajipa ujasiri, kuna saa unatamani kukata tamaa lakini ukipata riziki kidogo unapata nguvu ya kuendelea", alisema Bounako ambaye ameachia wimbo wake mpya wa Hip Hop unaoitwa bado tunapeta.