Tuesday , 16th Jun , 2015

Msanii wa muziki Dudu Baya ameshambuliwa vikali na wasanii wenzake na kupingwa kutokana na maneno yake aliyotoa kuhusu muziki unaofanywa hivi sasa.

Kufuatia kauli nzito ya msanii wa muziki Dudu Baya aliyoitoa katika mahojiano aliyofanya na kipindi cha Planet Bongo, kuwa wasanii wanaofanya muziki wenye mahadhi kutoka nje ya nchi ikiwepo kwaito na miondoko ya Afrika Magharibi ni sawa na mnyama 'nguruwe', mkali huyo ameshambuliwa vikali kupingwa kutokana na maneno yake hayo.

Kwa kujikumbusha tu, hivi ndivyo alivyosema Dudu Baya, akitoa kauli ya kuudhi kuwa wasanii hao ni sawa na mnyama nguruwe ambaye hana Kinyaa, akiwa na uwezo wa kujisaidia na kulala sehemu moja.

Madee kama moja ya mastaa ambao wana rekodi kadhaa za miondoko ya Kwaito, akatetea hatua yake hiyo na kumtaja Dudu Baya kama msanii aliye katika wakati mgumu kwa upande wa sanaa yake na msongo wa mawazo, na anayeweza kusema chochote kile ili kuvuta watu wamsikie.

Madee amesema kuwa, muziki hauna mipaka na unafanyika na kuzungumzwa mahali popote pale, na ukishapata nafasi hiyo inakuwa ni fursa nzuri ya kufanya biashara.

Vilevile kuhusiana na hili, Chegge naye kama moja ya mastaa walio na rekodi yenye mahadhi ya kwaito, ameiambia eNewz kuwa hawezi kusema chochote kuhusu alichokisema Dudu the Mamba.