Thursday , 8th May , 2014

Mwanamuziki wa Kenya, Daddy Owen ameendelea kuonesha moyo wake wa ukarimu kupitia taasisi yake ya hisani ya Malaika Trust, ambapo safari hii ameamua kujitolea kulipa gharama za masomo za binti mwenye tatizo la macho, ambaye anaitwa Dais Kangogo.

Akiwa analenga zaidi watu wenye ulemavu wenye jitihada za kujikwamua, Daddy Owen ameamua kumpatia binti huyu nafasi ya kupata elimu bora, kwaajili ya kumuwezesha kusimama mwenyewe na kuendesha mambo yake kwa kujitegemea katika siku za mbeleni.

Daddy Owen, pia anatambulika kwa mchango wake katika kumsaidia msanii wa muziki Denno ambaye ana ulemavu wa macho, kumpatia nafasi ya kuingia katika muziki na kuonesha kipaji chake cha ajabu, ambapo kwa pamoja walifanikiwa kutoa rekodi kali inayokwenda kwa jina Mbona.