Gabo Zigamba
Gabo ambaye pia ni mmoja kati ya washiriki wanaowania tuzo za EATV, alitoa somo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa akijibu maswali ya wanafunzi wa UDSM, katika kampeni ya 'Ready To Work' inayoendeshwa na Benki ya barclays ikiwa na lengo la kukabiliana na tatizo la ajira.
Gabo alisema endapo wasanii wataamua kuwa na umoja wenye nguvu, hakuna kitakachoharibika, na tasnia hiyo itapiga hatua kwa kiasi kikubwa kama ajira rasmi.
"Tasnia ya filamu inasuasua kwa kuwa wasanii tuna umoja wa nyumbu, tuko 20 lakini simba mmoja anatutoa jasho" Amesema Gabo
Akijibu swali kuhusu siri ya mafanikio yake na nani aliyemtoa, Gabo alisema kilichomfikisha hapo ni matumizi mauri ya akili zake na kwamba hakuna mtu yeyote aliyemsaidia huku akiwaasa wasanii wengine kuwa na matumizi mazuri ya akili zao ili kuisukuma mbele tasnia hiyo.
"Nisiwe mnafiki, matumizi mazuri ya akili zangu ndiyo yamenifikisha hapa, siwezi kusema kuna mtu ambaye amenipa mafanikio, katika tasnia ya movie tuna tatizo la matumizi sahihi ya akili, wengi hatujui jinsi ya kutumia akili zetu, tutakapojua kutumia akili zetu tutapiga hatua"
Gabo anawania tuzo hizo kupitia kipengele cha Muigizaji Bora wa Kiume.