Monday , 5th Dec , 2016

Nyota wa filamu nchini Tanzania aliyefanikiwa kuingia kwenye kinyang'anyiro cha Tuzo za EATV (EATV Awards) mwanadada Khadija Ally amefunguka na kuichana tasnia ya filamu nchini kuwa imejaa ubaguzi.

Khadija Ally

 

Khadija amefunguka hayo mwishoni mwa wiki akiwa na washiriki wenzake wa tuzo hizo katika ukumbi wa Nyerere Theatre 1 wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya ku'share' na wanafunzi mikakati ya kukabiliana na tatizo la ajira kupitia kampeni ya 'Raedy To Work' inayoendeshwa na Benki ya Barclays Tanzania.

Khadija aliyekuwa akijibu maswali ya wanafunzi, alisema kuwa wadau wengi wa bongo movie nchini wanapanga na kuchagua wasanii wa kuigiza (cast) kwa kuangalia uzuri wa sura na maumbile ili filamu zao ziuze badala ya kuangalia uwezo wa mtu.

Akizidi kufunguka, Khadija alisema waongozaji wengi hawatoi nafasi kwa waigizaji wenye umbo kama lake, ("Sina hata nyama") na ndiyo sababu aliamua kuigiza aina tofauti ya movie (Movie za action) zinazohusisha mchezo wa karate ambao amejifunza makusudi ili kuchezea movie.

"Nilipoona sipati nafasi ya kuigiza, nikashauriwa nitoke kivingine, nikaamua kujifunza karate ili nicheze movie za action maana ningelazimisha kucheza movie za kwenye masofa ningeonekana siwezi,,,,, Wasanii wengi wa movie hatupendani, na tumejawa na ubaguzi wa kuangaliana, tofauti na wenzetu wa bongo fleva ambao kila kukicha wanafanya kolabo" Amefunguka Khadija Ally.

Aidha kuhusu ubaguzi alitolea mfano wasanii walipoitwa Ikulu na Rais, na kujikusanya kwa misingi ya ubaguzi "nakumbuka kuna siku tulisikia wasanii wameitwa Ikulu, nilipowaona nikaona ni sura zilezile, nikajiulza inamaana wengine siyo wasanii?

Mwisho ameishukuru EATV kwa kuanzisha tuzo hizo, na kumfanya aweze kutambulika kwenye ramani ya movie nchini.

Khadija anawania tuzo za EATV katika kipengele cha muigizaji bora wa kike. kwa taarifa zote kuhusu tuzo na jinsi ya kupiga kura  ingia eatv.tv/awards

Tags: