Friday , 21st Sep , 2018

Muigizaji mkongwe wa filamu nchini, Jacob Stephen 'JB' amefunguka na kuitetea tasnia ya filamu nchini kuwa haijawahi kushuka hata mara moja kama baadhi ya watu wanavyosema, bali kilichotokea ni wasanii waliacha kutengeneza filamu hizo kwa muda.

Muigizaji mkongwe nchini Jacob Stephen 'JB.

JB ameeleza hayo alipokuwa anazungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam hii leo Septemba 21, 2018 na kusema kuwa watu wanashindwa kutofautisha kati ya kushuka soko na kutotengenezwa filamu na kupelekea kuona tasnia hiyo imekufa kwa sasa.

"Watu wanasema soko la filamu limeshuka huo ni uongo, filamu hazijashuka bali hazitengenezwi kabisa. Unajua kushuka ni kitu kingine na kutokutengenezwa kiti kingine kabisa. Hizo filamu mnazoziona mtaani zina kama miaka mitano filamu mpya ambazo zimetengenezwa mwaka huu na uliopita hazifiki hata sita", amesema JB.

Pamoja na hayo, JB ameendelea kwa kusema kuwa "watengenezaji wa filamu wamesimama, 'industry' sio kama wanatengeneza filamu mbovu bali watu hawatengenezi kabisa. Msiache kutukosoa kwa kila tukifanyayo, endeleni kufanya hivyo ili kusudi tuweze kuboreka zaidi kazi zetu".

Kwa upande mwingine, JB amesema kuwa kwa sasa ulingo wa filamu utainuka kivingine kwa kuwa wameweza kupata mkombozi katika kuuza kazi zao, hivyo hawataweza kuona hasara kuwekeza zaidi na kutoa filamu zilizokuwa na ubora ambao watanzania wengi walikuwa wanaulilia kwa miaka mingi.