Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania Mhe. William Lukuvi amesitisha zoezi la bomoabomoa kwa muda katika maeneo ya mabondeni na maeneo yaliyovamiwa na kujengwa kinyume cha sheria ili kutoa nafasi kwa watu waliojenga katika maeneo hao kuondoa wenyewe mali zao.
Wakiongea leo Jijini Dar es Salaam katika mkutano uliomjumuisha Waziri Lukuvu pamoja na Waziri wa Mazingira Mhe. Januari Makamba kwa pamoja wamesema kuwa watahakikisha kuwa sheria inafuatwa katika kubomoa maeneo yanayomilikiwa kinyume cha sheria.
Waziri Lukuvi amesema kuwa zoezi hilo limesitishwa mpaka ifikapo tarehe 5 Januari mwakani na kuwataka wale ambao wamejenga kinyume na utaratibu kubomoa wenyewe nyumba zao ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza wakati serikali itakapoamua kuvunja.