Wednesday , 28th Nov , 2018

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zenye madai kuwa Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako ametangaza viwango vipya vya ufaulu kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na sita.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mwasu Sware amesema kuwa Waziri Ndalichako hajawahi kutangaza kuwepo kwa viwango vipya.

"Taarifa ya namna hiyo ilishawahi kusambazwa mwaka jana na Wizara ilikanusha, Mheshimiwa Waziri hajatangaza na wala hajazungumza na chombo chochote kuhusu suala la kuwepo kwa viwango vipya", amesema Mwasu.

Aidha taarifa hiyo imeonya wasambazaji wa taarifa zinazosababisha taharuki kwenye mitandao ya kijamii, kuhakikisha kuwa zimethibitishwa na mamlaka husika ili kuepusha usumbufu.

Mwanzoni mwa wiki hii kumekuwa na taarifa zilizosambaa mitandaoni zikidai kuwa viwango vya ufaulu vya wahitimu wa kidato cha nne na sita zimebadilika.