Wednesday , 18th Jan , 2017

Waziri Mkuu ametoa siku nane kwa watu wote wanaomiliki silaha katika wilaya za Kilindi na Kiteto wazipeleke kwenye vituo vya Polisi ili zisajiliwe upya, na kuwataka wenye mitambo ya kutengezea bunduki kujisalimisha wenyewe haraka.

Bunduki

 Ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya za Kiteto na Kilindi katika kijiji cha Lembapili wilayani Kiteto, mkoani Manyara ambako kuna mpaka wa  wilaya hizo mbili.

Waziri mkuu ambaye alikuwa amekwenda kwenye eneo hilo kusuluhisha mgogoro wa mpaka kati ya wilaya hizo, amesema baada ya siku nane kumalizika Wakuu wa Mikoa wafanye operesheni maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume cha sheria achukuliwe hatua.

“Wakuu wa Mikoa fanyeni ukaguzi maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume na utaratibu achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria. Pia kuna watu wana mitambo ya kutengenezea bunduki hapa, nao pia waisalimishe haraka,” amesisitiza. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizugumza na  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi   (kushoto),  Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera wakiwa katika kijiji cha Lembapuli kilichopo kwenye mpaka  wa wilaya ya Kiteto na Kilindi  Januari 18, 2017. 

Katika hatua nyingine Majaliwa ameumaliza mgogoro wa mpaka wa ardhi baina ya vijiji vya wilaya za Kiteto na Kilindi uliodumu kwa muda mrefu huku akiwataka wanasiasa na viongozi wengine kutowavuruga wananchi na badala yake wawaongoze vizuri na kutoa maelekezo kwa mujibu wa sheria za nchi

Mgogoro huo ambao ulianza kusuluhishwa tangu mwaka 1997, umepata suluhu kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu na kuwajumuisha Wakuu wa Mikoa hiyo miwili, Wabunge wa Kiteto na Kilindi, wenyeviti wa Halmashauri na madiwani wa kata mbili za mpakani pamoja na wananchi wa kata hizo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akihutubia  mkutanao wa hadhaa katika kijiji cha  Lembapuli kilichopo mpakani mwa wilaya za Kilindi na Kiteto alikokwenda kutatua mgogoro wa  mpaka  Januari 18, 2017.