Saturday , 24th Sep , 2016

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, amewataka watumishi wa umma nchini kuwa tayari kwenda kufanya kazi kokote watakalopangiwa na Serikali kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Mkunguni wilayani Mafia, ambapo amesema moja ya wajibu wa watumishi wa umma ni kuwatumikia na kuwahudumia Watanzania sehemu yoyote walipo, ili kuwaletea maendeleo na atakayeshindwa ni vema akatafuta shughuli nyingine nje ya ajira za Serikali.

Alisema Serikali ya Awamu ya tano imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.

Waziri Mkuu alisema kila awamu inakuwa na mkakati wake, watumishi wa umma wanatakiwa kubadilika na kufanya kazi kutokana na awamu iliyoko madarakani inavyotaka.