Tuesday , 24th May , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo anahudhuria Mkutano wa 51 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika nchini Zambia ikiwa ni kwa niaba ya Mhe. Rais, Dk. John Pombe Magufuli.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awasili Lusaka, Zambia, Kwenye Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Mkutano huo ambao utafunguliwa na Rais wa Zambia, Edgar Lungu utajadili masuala ya Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Pia utahudhuriwa na Marais Idriss Deby wa Chad, Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya huku Nigeria ikiwakilishwa na Makamu wake wa Rais, Yemi Osinbajo na Msumbiji iitawasilishwa na Waziri wake Mkuu, Carlos Agostinho do Rosário.

Watu maarufu waliothibitisha kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Kofi Annan, Ashish Thakkar, John Kufuor, Mary Robinson, Mo Ibrahim, Nancy Lee, Ngozi Okonjo-Iweala na Tony Elumelu.

Mkutano huo utakaofanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mulungushi (Mulungushi International Conference Centre) utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 5,000 kutoka nchi 54 ambao ni wanachama wa benki hiyo, washiriki kutoka nchi 26 ambazo si za bara la Afrika (non-regional member countries), wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa asasi za kiraia.

Wengine ni Mawaziri wa fedha, biashara na uchumi na wataalamu kutoka vyuo vikuu.

Waziri Mkuu amefuatana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, wachumi kadhaa pamoja na wataalamu wa sekta ya fedha.