
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wakati wa ufunguzi wa safari za majaribio katika reli ya kisasa
Katika uzinduzi wa safari hiyo, Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa serikali imeanza mchakato wa ununuzi wa vichwa 22 vya treni, mabehewa 1,430 ya mizigo na Mabehewa 60 ya Abiria vitakavyotumika kwenye uendeshaji wa Reli ya kisasa ya SGR ambayo ujenzi wake unaendelea.
Reli ya SGR awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 56, ukisimamiwa na Yapi Merkez inajenga na awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora Mkoani Singida ikiwa imefikia asilimia 52 zote zikiwa na urefu wa zaidi ya kilomita 722 na zinajengwa kwa gharama ya fedha za ndani shilingi Trilioni 7.2.
Injinia Kamwelwe amesema mpango wa sasa wa Serikali ni kuwa na Seti tano za Treni za SGR zitakazokuwa na behewa nane za abiria
“Ndugu zangu Watanzania, leo hii tumezindua majaribio ya njia ya reli yetu, hii inamaana kwamba tupo katika mipango ya kuhakikisha reli inakamilika kwa wakati, tumetembea kilomita 20 za majaribiop, reli ni salama kabisa, haina kikwazo, sasa tumeanza mchakato wa kununua vichwa vya treni 22 na mabehewa yake 60 ya Abiria na 1,430 ya Mizigo” amesema Waziri Kamwelwe.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania TRC Masanja Kadogosa amesema zoezi la majaribio ya awali ya treni ya wahandisi ni hatua muhimu ya kuhakikisha reli hiyo inapitika bila kikwazo kwani inakagua na kuimarisha miundombinu.