Baadhi ya wazee wilayani Butiama katika mkutano wao na mkuu wa wilaya hiyo.
Wakati bunge la katiba likitarajia kuanza vikao vyake mwezi ujao, wazee kutoka koo nane za kabila la wazanaki katika wilaya ya Butiama mkoani Mara, wamelaani vikali kauli za kejeli na matusi zinazoelekezwa kwa waasisi wa muungano hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Abeid Aman Karume kwa kile ambacho wamekisema ni kukosa heshima kwa mchango mkubwa wa waasisi hao.
Wazee hao wametoa tamko hilo wakiwa makao makuu ya wilaya ya Butiama mbele ya mkuu wa wilaya hiyo, ambapo wamesema kuwa hayati mwalimu Julius Nyerere licha ya kuzaliwa katika kijiji cha Butiama mkoani Mara hakuwa mbinafsi katika utawala wake hivyo kauli la kejeli na matusi dhidi yake zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba ni kumkosea heshima.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Butiama Bi Angelina Mabula, akijibu tamko hilo la wazee wa Butiama amesema watanzania leo wanapaswa kutambua wametoka wapi, wapo wapi na wanakwenda wapi na pia umuhimu wa waasisi hao.