Monday , 7th Mar , 2016

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo, amewasimamisha kazi wauguzi 11 katika hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure, pamoja na ya wilaya ya Nyamagana, Butimba kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo kusababisha vifo vya watoto pacha na mjamzito.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo.

Akiwataja waathirika hao wa matukio ni mwanamama Susaza John, ambae alijifungulia kwenye beseni watoto mapacha katika hospitali ya Butimba, na watoto kufariki pamoja na Pendo Masanja ambae alijifungua mapacha waliofariki na yeye kupoteza maisha.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema uamuzi wa kuwasimamisha kazi watumishi hao wa afya umefanyika baada ya kugundua uzembe mkubwa wa kitaaluma pamoja na lugha chafu zilizotumika wakati wa kuwahudumia wagonjwa.

Akizungumza na madaktari na wauguzi katika hospitali ya Sekou toure,Mulongo amesema matukio hayo yameleta taswira mbaya kwa mkoa wa Mwanza kutokana na ukweli kuwa shughuli zinazofanywa na taasisi hizo zina lengo la kuokoa maisha ya watu.

Akizungumza baada ya tukio hilo dada wa Marehemu Pendo Masanja, Deborah Khamis amesema kifo cha ndugu yake kimetokana na uzembe wa wauguzi na madaktari na kudai kuwa baada ya kufika hospitali alicheleweshwa kupewa huduma.