Saturday , 4th Mar , 2017

Jumla ya watumishi wa umma 2,059 wamekwisharipoti Dodoma katika awamu ya kwanza ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati akikabidhiwa uenyekiti wa CCM, Julai 22, mwaka jana.

Kassim Majaliwa - Waziri Mkuu

Awamu ya kwanza ya Serikali kuhamia Makao Makuu Dodoma inajumuisha Mawaziri na Manaibu wao, Makatibu Wakuu na manaibu wao, baadhi ya wakurugenzi pamoja na wasaidizi wachache.

Hayo yamebainika katika Kikao cha Kazi cha Mawaziri na Naibu Mawaziri kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hazina mjini Dodoma chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wakiwasilisha taarifa hizo, Mawaziri hao wote wamethibitisha kwamba tayari ofisi zao na wao wenyewe wameshahamia Makao Makuu Dodoma pamoja na watumishi wao wote walioko kwenye awamu ya kwanza na wameahidi kukamilisha kuhamisha waliosalia katika awamu nne hadi sita kulingana na ratiba ya Serikali.

Aidha, Waziri Mkuu amesema baada ya Serikali kukamilisha ratiba ya kuhamia Makao Makuu Dodoma, Jiji la Dar es Salaam litabakia kuwa Jiji la kibiashara na wamepanga kuendelea kuendelea kuliboresha ili shughuli hizo zifanyike kwa ufanisi zaidi