Tuesday , 1st Dec , 2015

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawafikishe katika mamlaka husika watu wanaowakamata ili sheria ichukue mkondo wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,SACP Ahmed Msangi

Kauli hiyo ameitoa baada ya watu wa tatu kuuawa na wananchi wenye hasira katika matukio matatu tofauti jijini Mbeya likiwemo la mzee mmoja mwenye umri wa miaka 79 kukutwa ameuawa na wananchi hao kwa tuhuma za uchawi.

Kamanda Msangi amesema tukio la kwanza limetokea tarehe 30.11.2015 majira ya saa 11 jioni kijiji cha Mkunywa, kata ya Madibira, tarafa ya Rujewa, wilayani Mbarali ambapo mtu mmoja mkazi wa kijiji cha iIenzana aitwaye Niko Chaula [30], aliuawa kwa kupigwa na kundi la wananchi na kisha mwili wake kuchomwa moto.

Inadaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo ni kulipiza kisasi kutokana na tuhuma za marehemu kuhusika katika tukio la kupora pikipiki T.852 DAT aina ya Yamaha mali ya Aidan Waya [19], mkazi wa Isoko na kumjeruhi kwa kumchoma kisu.

Katika tukio la Pili mzee mmoja mkazi wa kijiji cha Ilolo, aitwaye Benard Buja [79], alikutwa ameuawa nyumbani kwake na watu wasiofahamika kwa kukatwa panga shingoni na kisha mwili wake kutupwa kwenye shamba mali ya Thomas Mwamakasi.

Inadaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina, kwani marehemu alikuwa anatuhumiwa kuwa ni mchawi kijijini hapo.

Na katika tukio la tatu mtu mmoja mkazi wa kijiji cha Ihenzana aitwaye niko chaula [30], aliuawa kwa kupigwa na kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi kisha mwili wake kuchomwa moto.