Saturday , 31st Jan , 2015

ASKARI mmoja wa wanyama pori na msaidizi wake wameuawa kwa kupigwa mawe, mapanga, marungu na nondo na wananchi katika kijiji cha Namonge Wilayani Bukombe Mkoani Geita wakituhumiwa kuwa majambazi.

Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu

ASKARI mmoja wa wanyama pori na msaidizi wake wameuawa kwa kupigwa mawe, mapanga, marungu na nondo na wananchi katika kijiji cha Namonge Wilayani Bukombe Mkoani Geita wakituhumiwa kuwa majambazi na tayari watu 24 wanashikiliwa akiwemo Afisa mtendaji wa kijijij hicho.

Tukio hilo limetokea jana jioni baada ya wananchi hao kuhamasishana wakakusanyika na kuivunja ofisi ya Serikali ya kijiji hicho walimokuwa wamehifadhiwa kwa usalama wao na Afisa mtendaji wa kijiji hicho Andrea Malise wakati akifanya jitihada za kuwasiliana na Polisi ili wafike eneo la tukio kuwaokoa watu hao bila ya mafanikio.

Akithibitisha leo asubuhi kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa wilaya ya Bukombe Amani Mwenegoha amesema watu 24 akiwemo Afisa mtendaji wa kijiji hicho wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi mkali unaendelea.

''Ni kweli Askari na msaidizi wake wa wanyama pori wameuawa na majina yao yatapatikana baadaye wameuawa katika mazingira yanayodaiwa na tayari kikao cha kamati ya ulinzi na usalama wilaya kitakutana dharura leo mchana kujadili tukio hilo ..kwani vitendo vya aina hii haviwezi kuvumiliwa vya kujichukulia sheria mikononi''alisisitiza Mwenegoha.

Wakisimulia chanzo cha tukio hilo kijijini hapo baadhi ya wananchi wamedai waliwaona jana alasiri watu watano mmoja wao akiwa na silaha aina ya SMG lakini baadaye waliwaona wakipita na baada ya muda kupita waliouawa walirudi na kuingia Bar wakiwa na pikipiki lakini bila silaha kutokana na kuonekana wageni ndipo wanakijiji walianza kuhoji na kuwasiliana juu ya watu hao.

Pasipo subira inadaiwa wananchi walianza kuwatupia mawe na ndipo Afisa mtendaji wakijiji hicho Alipoingilia kati na kuwaweka katia ofisis yake kukwepa vipigo kutoka kwa wananchi huku akiwalsaina na polisi wa kituo cha Lunzewe kilichopo umbali kama kilometa 30 ambapo wananchi walianza kushambulia jengo la ofisi na kulivunja milango na madirisha.

Baada ya kufanikiwa kulivunja jengo la ofisi ya serikali ya kijiji waliweza kuwashambulia watu hao hadi kuwaua na kisha kuchukua kila kitu walichokuwa nacho ikiwemo fedha walizokuwa nazo mfukoni na kuiharibu pikipiki waliyokuwa nayo wakigawana vifaa vyake zikiwemo tairi na taa na kuacha frame peke yake kabla ya Askari polisi kufika eneo la tukio na kutawanyika.

Chanzo cha mkasa huo kinadaiwa Askari hao wawili waki wamevaa kiraia wakiwa na pikipiki baada ya kurudi tena wakiwa bila ya wenzao waliokuwa na Bunduki waliingia Baa na kuanza kupata kinywaji na ndipo wananchi walipoanza kuwasiliana kuhoji juu yao na kisha kuhamasishana kuwashambulia kwa madai huenda walikuwa ni majambazi.

Habari zaidi kutoka eneo la tukio na kuthibitshwa na Afisa mtendaji wa kata ya Namonge Charles John amesema Askari hao waliuawa baada ya ofisi ya serikali ya kijiji kuvunjwa na wananchi na kisha kuanza kuwashambulia watu hao wakidai kuwa ni majambazi kabla ya kutambuliwa na Askari wanyama pori waliofika eneo la tukio na kudai walikuwa ni Askari wa wanyamapori wenzao.

''Askari hao kufika kijijini ..bila kuripoti ofisi ya kijiji wala Kata kunaweza kuwa kumechangia kwa kiasi kikubwa kutokea mkasa huo kutokana na ukweli uongozi wakijiji na kata haukuwa na taarifa ya kuwepo na ujio wa Askari hao hivyo kushindwa kuchukua hatua mapema hii ni hatari sana kuingia katika kijiji bila taarifa kinyemela'' alidai John.

Hofu ya wananchi inadaiwa kuchangiwa na kuwepo kwa matukio ya uhalifu mara kwa mara katika ukanda huo likiwemo la mnada wa ng'ombe kuvamiwa na watu wenye silaha Januari 16 na Watu wengine wenye silaha kuingia katika kijiji cha Ilyamchele Januari 19 na kuwateka wanakijiji baada ya kuwakirimu.

Pamoja na kuwepo mazingira na utetezi huo imedaiwa kuwa serikali isipochukua hatua kali kukomesha vitendo vya ubebaji sheria mikononi kuna hatari ya kuibuka tabia ya kulipizana kisasi na kubambikiziana tuhuma na hivyo kukosekana kwa utawala wa sheria na kikatiba na kuuawa wasio na hatia.

Kufuatia tukio hilo mamia ya wanaume wanadaiwa kukimbia kaya zao na kutokomea kusikojulikana kutokana na kuhofia kukamatwa na hivyo familia kubakiwa na wanawake, vikongwe na walemavu pake yao.