Mmoja wa Watoto kutoka shule ya Msingi Mariado Primary, Gifti Gervas
Aidha watoto hao wamesema kuwa mitazamo hasi na mila potofu zinazoendana na ushirikina zimekuwa kikwazo na tishio kwa jamii ya watu wenye albinism ambao wakipata fursa ya elimu wanaweza kuisaidia jamii kuondokana na changamoto lukuki zinazoikabili kupitia uwezo na vipaji walivyonavyo.
Wakizungumza katika maadhimisho ya siku ya haki za binadamu yaliyofanyika katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyoko jijini Arusha, watoto hao kutoka shule ya msingi Mariado, Gifti Gervas ameiomba serikali na mashirika ya haki za binadamu kuhakikisha yanawalinda ili waweze kupata haki ya kupata elimu bora pamoja na haki ya kuishi kuishi.
Mtoto Saida Alhaji ameiomba serikali iboreshe mazingira ya watoto wenye albinism hasa wale waishio vijijini ili waweze kupata elimu na kuwa msaada kwa jamii.
Kwa upande wake kamishna wa tume ya haki za binadamu (CHRAGG) Mohamed Khamis amesema kuwa tume yake imekuwa ikifuatilia kwa makini suala la ulinzi wa albino na kusikitishwa na mauaji ya albino ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kuchukua sura ya ushirikina jambo ambalo wanalilaani vikali na kuweka msukumo wa kumaliza tatizo hilo.
Mauaji ya watu wenye albinism yamekuwa yakitia dosari taswira ya taifa hasa katika masuala ya kimataifa ya haki za binadamu hivyo ni jukumu la kila mtu pamoja na serikali kuhakikisha kuwa mauaji ya albino pamoja na vikongwe yanakomeshwa ili kuwa na jamii inayoheshimu haki za binadamu.