Tuesday , 4th Oct , 2016

Watanzania wametakiwa kupenda na kuvienzi viwanda vidogo na kujivunia bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivyo kwa kuzitumia ili kujenga uchumi wa nchini kupitia viwanda hivyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo(SIDO), Prof. Silvester Mpanduji.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO), Prof. Silvester Mpanduji wakati akifunga maonesho ya wenye viwanda vidogo na kati nyanda za juu kusini Mkoa Mbeya.

Prof. Mpanduji amesema kuwa kuzalisha na kutumia bidhaa za ndani ndiyo njia pekee ya kufanikisha kuifikisha nchi kwenye uchumi wa viwanda hivyo maendeleo katika sekta hiyo ni muhimu.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa bila teknolojia nyepesi na rahisi ya kukidhi mahitaji ya soko la ndani itakuwa vigumu kumudu ushindani katika kipindi hiki cha utandawazi.

Aidha amesema kuwa katika kuboresha sekta hiyo wajasiriamali wanahitaji utaalam wa kutosha wa kubuni na kutayarisha michanganuo ya miradi inayokubalika na mabenki pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa masharti nafuu kutoka taasisi za fedha.