Wednesday , 27th Apr , 2016

Kushuka kwa gharama za nishati ya gesi imetajwa kuwa ni fursa muhimu kiuchumi ambayo Watanzania wametakiwa kuitumia ili kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambao taarifa za kitaalamu zinaonyesha kuwa huchangia kuharibu mazingira.

Mtaalamu wa ufundi na biashara ya gesi kutoka eneo la Bamaga jijini Dar es Salaam Bw. Salim Nassor Abdallah, ametoa wito huo katika mahojiano na hotmix, iliyotaka kufahamu sababu ya kuwepo kwa Watanzania wanaotumia mkaa na kuni kama nishati yao ya matumizi ya nyumbani na katika biashara.

Katika maelezo yake, Bw. Nassoro amesema kiwango cha chini ya gharama za gesi kwa mwezi hakizidi fedha za Tanzania shilingi elfu arobaini tofauti na kuni na mkaa ambao mtumiaji hulazimika kulipia kati ya shilingi elfu sabini na tisini kwa mwezi.

"Nikiwa kama mtaalamu wa ufundi na biashara ya gesi, nawashauri Watanzania wenzangu waanze kutumia gesi na kuachana na kuni na mkaa kwani vinaharibu mazingira," amesema Bw. Nassor huku akiwataka waachane na mtazamo kuwa gesi inauzwa kwa gharama ya juu wakati ukweli ni kwamba kuni na mkaa ndio zinazogharimu kiasi kikubwa cha pesa,"