Thursday , 21st May , 2015

Zoezi la uandikishaji wapigakura linalotarajiwa kuanza manispaa ya Tabora leo, huenda likaingia dosari kutokana na upungufu wa kadi za kupigia kura na uchache wa vituo vya kujiandikisha.

Akizungumza na Ea Radio leo, msimamizi wa uchaguzi wa manispaa hiyo, Frank Mkoga, anasema manispaa hiyo ina jumla ya wananchi wanaostahili kupiga kura 130,686, lakini hadi sasa kadi zilizopelekwa na tume ya taifa ya uchaguzi ni 50,000 wakati zoezi la uandikishaji linaanza leo.

Mkoga amesema lengo ni kuweka vituo 295 vya kujiandikisha, lakini cha kushangaza tume imepitisha vituo 221 tu.

Mbali ya kasoro hizo pia mashine za kielekroniki za kuandiklishia wapiga kura (BVR) zilizopo ni 54 kwa ajili ya kazi ya zoezi hilo, hali inayoonesha wazi zoezi hilo linaweza kukwama ukizingatia uzoefu wa waandikishaji wamepewa mafunzo ya siku mbili tu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Christopher Msuka, amesema kuna changamoto nyingi za kuanza uandikishaji huo kwa wananchi kutokana na wengi wao kutofahamu siku ya uandikishaji huo.

Msuka anasema vituo vya kujiandikisha ni vichache kiasi kwamba wananchi wa vijijini watatembea umbali mrefu sana kutafuta vituo vya kujiandikishia na wakikuta watu ni wengi wakiondoka hawarudi tena.

Mwenyekiti huyo alisema tume inatakiwa kutumia busara kuhakikisha watu wote wanapata haki ya kujiandikisha kwenye daftari hilo.