Wednesday , 7th Sep , 2016

Watu wenye matatizo ya kutosikia (Viziwi) wameitaka serikali kutatua changamoto ya kukosekana kwa njia rafiki ya mawasiliano itakayowawezesha kusikia masuala mbalimbali yanayofanyiwa maamuzi na serikali hususani katika uwasilishwaji wa hotuba za Rais

Naibu Waziri anayehusika na watu wenye ulemavu, Dkt Abdallah Possy

Akiongea na East Africa Television, leo jijini Dar es Salaam wakati wakipatiwa mafunzo ya ulipaji kodi kwa viziwi zaidi ya 60 kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania Mwenyekiti wa Miradi ya Viziwi Tanzania Bw. Joseph Hizza amesema imekuwa vigumu kwa viziwi kupata taarifa muhimu kwa wakati kutokana na taarifa hizo kukosa wakalimani wa lugha za alama.

Bw. Hizza amesema imefika wakati sasa kundi hilo likumbukwe kwani athari za kukosa taarifa muhimu zinawaathiri kwa namna mbalimbali na kwamba ni vyema kukawepo na mkalimani wakati wa kuwasilisha hotuba zote za Rais.

“Hotuba za Rais tunge penda ziwe na wakalimani wa lugha za alama kwani ni vigumu kwetu kutambua ni nini kinaendelea,” alisema Bw. Hizza.

Amesema kupata habari ni jambo la Kikatiba hivyo wasio sikia wamekosa fursa hiyo kwa muda mrefu jambo ambalo linapelekea kushindwa kuendesha shughuli zao za uzalishaji kikamilifu.

Afisa Msaidizi Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Bw. Chuwa Sirwa amesema TRA imeamua kutoa elimu ya kodi kwa viziwi ili kuondokana na changamoto ya mawasiliano pindi wanapotembelea kwenye biashara zao.