Wednesday , 26th Aug , 2015

Wananchi wakiwemo wafanyabiashara wadogo wadogo wa vyakula mkoani Morogoro wameishauri mamlaka husika kuwatafutia maeneo ya kufanyia biashara zao wakati huu wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Mmoja ya Wafabiashara wa vyakula mjini Morogoro ambae ameziomba mamlaka kuwatafutia sehemu salama

Maoni hayo yamekuja baada ya halmashauri ya manispaa ya Morogoro kupiga marufuku uuzaji holela wa vyakula na kuwakamata wanaokwenda kinyume na agizo hilo, nia ikiwa ni kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu, hatua ambayo imefanya wananchi wengi hasa wa kipato cha chini kukosa maeneo nafuu ya kula.

Mganga mkuu wa manispaa ya Morogoro Dkt. Nicholaus Chiduo amesema wameweka mikakati mbalimbali kukabiliana na kipindupindu,ikiwemo kudhibiti uuzaji holela wa vyakula,utoaji wa elimu na kukagua magari yanayobeba maji na wamefanikiwa kupunguza ugonjwa huo kwa kubakiza wagonjwa 18 tu waliolazwa hadi sasa toka 48 waliugua.

Hapo jana Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema hadi kufikia jana watu 7 wamefariki kwa ugonjwa huo kwa Morogoro na Dar es Salaam huku watu 294 wakiugua ugonjwa huo ambapo baadhi yao wameruhusiwa.