Sunday , 1st Nov , 2015

Viongozi wa madhehebu mbalimbali yaliyopo wilayani Meatu mkoani Simiyu wamewaomba wanasiasa ambao hawakubahatika kushinda katika nafasi za udiwani na ubunge kuondoa tofauti zao na badala yake waungane katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Meatu bw Erasto Sima

Hayo wameyasema katika tathimini ya zoezi la uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani katika majimbo ya Meatu na Kisesa baada ya kukutana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Meatu ili kuweza kubaini kasoro zilizojitokeza na kuboresha katika chaguzi zingine zijazo.

Wamesema kuwa uchaguzi umeisha hivyo wanasiasa waungane pamoja katika kulijenga taifa la Tanzania katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kila mmoja kutokuwa na kinyongo chochote.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Meatu Bw. Erasto Sima amevipongeza vyombo vya ulinzi kwa kazi nzuri ya kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa katika kipindi chote cha zoezi la kupiga kura na hatimaye matokeo.

Walioshiriki katika tathimini hiyo ni vyama vya wafanyakazi,makundi maalum ya ,wenye ulemavu wa ngozi viungo ,mwakilishi wa wanawake na vijana huku wakisema kuwa wameridhishwa na hali ya utulivu iliyoonyeshwa wakati wa zoezi la kupiga kura .