Thursday , 12th Nov , 2015

Wakati serikali ikisema elimu bure kuanzia mwaka ujao mkuu wa shule ya msingi Matiganjola iliyopo halmashauli ya wilaya ya Njombe, amewarudisha wanafunzi nyumbani kufuata michango kwa ajili ya chakula cha mwaka 2016.

Afisa elimu mkoa wa Njombe Bw. Said Nyasiro akisoma taarifa ya elimu kimkoa.

Wakizungumza kwa jazba baadhi ya wazazi wa watoto waliorudishwa nyumbani, wamesema kuwa wameshangaa kuona kuwa watoto wao wanarudishwa kwa sababu ya michango wakati michango ya chakula kwa mwaka huu inatosha na kukubaliana kupeleka michango wanapompeleka mtoto mwezi wa kwanza.

Wazazi hao wamesema kuwa wanashangazwa na kitendo cha watoto wao kurudishwa kwa ajili ya michango ya mwaka ujao wakati mwaka huu haujaisha huku wazazi wengine wakisema kuwa wamefanikiwa kulipa michango yote kwa mwaka huu lakini bado wanashangaa watoto wao kurudi nyumbani.

Akijibu tuhuma hizo mwalimu mkuu wa shule ya hiyo, Athanasio Ulime amekiri kurudisha watoto hao nyumbani kwa ajili ya kuwakumbusha wazazi wapeleke michango ya mahindi ya mwaka 2016 kutokana na baadhi yao kushindwa kuwasilisha michango hiyo kwa wakati ambapo amesema lengo ni kuwahimiza wazazi wapeleke michango hiyo.

Naye mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Matiganjola Jactan Mwani akizungumzia suala hilo amesema suala hilo walikubaliana kwenye mkutano wa hadhara wa Oktoba 13 huku akisema wananchi wanaendekeza siasa hata muda ambao siasa zimekwisha

Kwa upande wake afisa elimu shule za msingi wilaya ya Njombe Catherine Kihaule amekanusha kupokea taarifa za kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi wa shule ya msingi matiganjola na kwamba hakuna mwalimu anayeruhusiwa kuwafukuza wanafunzi kwa kosa la kutopeleka michango badala yake serikali za vijiji, kamati za shule pamoja na wazazi wahusike.

Kufuatia kufukuzwa kwa wanafunzi na kurudi nyumbani wazazi wa kijiji hicho waliandamana kupinga hatua hiyo ya walimu kuwafukuza watoto wao shuleni na kuacha masomo.