Tuesday , 28th Apr , 2015

Chama cha wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani nchini Tanzania TABOA, kimetangaza mgomo mwingine nchi nzima ikiwa ni hatua ya kupinga nauli mpya za mabasi zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini SUMATRA.

Abiria wakiwa katika pilika pilika zikiendelea katika stendi ya mabasi ya kwenda mikoani ya Ubungo.

Akizungumza jana Jijini Dar es Salam Katibu Mkuu wa TABOA, Ernea Mrutu amewataka mawakala kutokatisha tiketi kuanzia leo mpaka hapo SUMATRA itakapotoa taarifa za kuruhusu nauli ya zamani ziendelee kutumika.

Mrutu ametoa taarifa hiyo wakati wa majumuisho ya mkutano mkuu wa dharura uliojumisha wadau wa usafirishaji ambao ulikua na ajenda tatu ambazo ni ajali za Barabarani, Nauli mpya zilizotangazwa na Sumatra, madaraja ya mabasi na vituo vya kubadilisha madereva wanaokwenda umbali mrefu.

Mrutu amesema iliyotolewa na SUMATRA kushusha nauli kutokana na bei ya mafuta kushuka sio kigezo muhimu bali ni shinikizo kutoka kwa wanasiasa.

Kuhusu ajali za barabarani amesema kutokana na kukithiri kwa ajali za mabasi wanakubaliana na utaratibu uliowekwa na serikali wa madereva kubadilishana wanaokwenda masafa marefu katika vituo ambavyo vitatengwa ili kupunguza ajali hizo.